Ufahamu Kiundani Ugonjwa Wa Kaswende
Kaswende ni ugonjwa unaoambukiza haraka sana, mara nyingi kwa kufanya ngono. Ugonjwa huu huenezwa kwa kugusa moja kwa moja mchubuko wa kaswende (syphilitic sore) uliopo kwenye ngozi, au kwenye ngozi laini zenye majimaji za ukeni, kwenye sehemu ya haja kutolea haja kubwa, na midomo.
Kwa hiyo njia kuu ambayo husabaisha kuenea kwa ugonjwa huu ni kupitia ngono ya kawaida, ya kutumia midomo na ile ya kinyume na maumbile. Mara chache ugonjwa huu huweza kuambukiza kwa kubusiana au kugusana miili. Pamoja na kuwa ugonjwa huambukiza kupitia michubuko, mara nyingi michubuko hatarishi haitambulikani.
Mtu aliyeambukizwa huwa hajielewi na hivyo kumwambukiza mpenzi wake.
Kaswende haiambukizi kwa kuchangia vyoo, vitasa vya milango, mabwawa ya kuogelea, kuchangia nguo au vyombo vya chakula.
Kaswende husababishwa na bakteria aitwaye Treponema pallidum, ambaye pia huitwa spirochetes kutokana na umbo lake la mzunguko. Viumbe hawa hujipenyeza kwenye ngozi laini inayotanda midomo au sehemu nyeti.
Mwanamke mwenye mimba na ugonjwa huu anaweza kumwambukiza mtoto aliye tumboni kupitia placenta au wakati wa kuzaliwa. Aina hii ya kaswende huitwa congenital syphilis, na inaweza kusababisha kujifungua mtoto mfu au mtoto akafa muda mfupi baada ya kuzaliwa.
Watoto wengi hawaonyeshi dalili wanapozaliwa. Baadaye watoto huota vijipele, hupata matatizo ya meno, na kubonyea kwa mfupa wa pua – hali inayoitwa saddle nose, kuwa viziwi, kuwa na watoto wa jicho na kifafa.
Ugonjwa wa kaswende hugawanywa katika hatua na kila hatua ikiwa na dalili tofauti, lakini wakati mwingine hakuna dalili zitakazojitokeza kwa miaka mingi.
Uambukizaji unatokea kwenye hatua ya kwanza, ya pili na mara chache mwanzoni mwa hatua ya latent phase.
Hatua Ya kwanza Ya Kaswende – Primary Syphilis
Kaswende huanza kama mchubuko mmoja (au zaidi ya mmoja) mgumu usio na maumivu unaojulikana kama chancre kwenye sehemu za siri, kwenye mdomo, au kwenye ngoz,i siku 10-90 (wastani wa miezi 3) baada ya maambukizi.
Mchubuko huu unaweza kubaki hapo bila kuleta usumbufu kwa kipindi kirefu na hata maiaka mingi. Mchubuko huu wa mviringo hutokea kwenye eneo la maambuikizi. Hata bila ya tiba yo yote, mchubuko huu unaweza ukapona wenyewe bila kuacha kovu katika wiki sita.
Hatua Ya Pili Ya Kaswende – Secondary Syphilis.
Hatua ya pili inaweza ikadumu kwa mwezi mmoja hadi miezi sita ikianza kama wiki sita hadi miezi sita baada ya maambukizi. Katika hatua ya pili, vijipele huota mara nyingi vikianzia mgongoni na kuenea mwili mzima, pamoja na kwenye viganja vya mikono na kwenye nyayo. Vijipele hivi huwa vya mviringo vyenye rangi nyekundu au vyenye wekundu wa kahawia.
Michubuko inayofanana na chunjua hutokea kwenye sehemu za midomo na mkundu. Vile kutatokea maumivu ya misuli, homa, kukauka koo, kuvimba tezi, kupunyuka nywele, kukonda na uchovu wa mwili.
Latent Syphilis
Kama tiba ya kaswende ya hatua ya pili haitatolewa, ugonjwa utaendelea kwenye hatua iitwayo latent stage. Katika hatua hii inayoweza kudumu kwa miaka kadhaa, mwili utautunza ugonjwa bila kuonyesha dalili zo zote. Pamoja na kuwa hakuna dalili zo zote zitakazoonekana, ugonjwa huu unaweza kuendelea kwenye hatua ya mwisho.
Hatua Ya Tatu Ya Kaswende – Tertiary syphilis
Asilimia 15 ya watu ambao hawakupata tiba kwenye hatua ya pili ya kaswende watapata kaswende ya hatua ya tatu – tertiary syphilis. Hatua hii inatokea miaka 10 hadi 30 baada ya dalili za mwanzo za kaswende. Dalili za kaswende za hatua hii ni pamoja na kushindwa kumudu matumizi ya viungo vya mwili, ganzi, upofu, ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu, madhara kwenye moyo na mishipa ya damu, madhara kwenye ini, mifupa na maungio ya mifupa. Kifo huweza kutokea kutokana na uharibifu wa viungo vya mwili.
Kuwahi kumpa tiba mgonjwa wa kaswende ni muhimu kwani kuchelewa kunaweza kumletea madhara makubwa ya mwili au kifo. Kama ugonjwa haujazidi mwaka mmoja, mara nyngi dozi moja ya ya penicillin hutosha. Kaswende iliyoendelea kwenye hatua nyingine, dozi nyingine zitahitajika.
0 comments: