Fangasi Sehemu za Siri za Mwanaume



Watu wengi wanaamini kuwashwa sehemu za siri kunasababishwa na fangasi tu, ndiyo maana nimepata maswali ya wasomaji juu ya matibabu na jinsi ya kujikinga na fangasi kwa kuwa wanaamini muwasho unaowasumbua kwa muda mrefu ni matokeo ya maambukizi ya fangasi. 

Watu wanapaswa kufahamu kuwashwa sehemu za siri kunaweza kuwa dalili ya maradhi fulani ndani ya mwili wako pengine isiwe ni fangasi na ikawa ni mzio (allergy) tu. 

Mara nyingi muwasho sehemu za siri unaosababishwa na kitu huisha wenyewe kitu hicho kikiondolewa. Kuondolewa kwa kitu hicho kunatia ndani matibabu sahihi na kuendelea na njia bora za kujikinga kutopata maambukizi tena. Vitu vingine vinavyosababisha muwasho huhitaji matibabu ya hali ya juu zaidi. Ikiwa unawashwa kwa muda mrefu ni vyema kuzungumza na daktari. Kukaa na ugonjwa kwa muda mrefu kunaweza sababisha ugonjwa kusambaa mwilini na kuongeza hatari ya kifo. 

Nini husababisha Muwasho Sehemu za Siri za Mwanaume? 
Kuwashwa uume au sehemu zingine za siri za mwanaume husababishwa na sababu zile zile zinazosababisha muwasho sehemu nyingine za mwili. 

Maradhi ya fangasi husababisha muwasho kwa wanaume wengi, sababu nyingine ni kama ugonjwa wa upele (scabies), kuwepo kwa chawa, mzio na maambukizi mengine ya bakteria. Maambukizi hasa ya magonjwa ya zinaa ndio chanzo kikuu cha kuwashwa uume. 

Fangasi sehemu za siri za mwanaume ni nini? 
Maradhi ya fangasi (Candidiasis) husababishwa na vimelea viitwavyo Candida albicans. Vimelea hivi hushambulia jinsia zote ingawa hushambulia sana jinsia ya kike kutokana na maumbile yao ya sehemu za siri kuwa na unyevunyevu kitu kinachosababia wao kuathiriwa zaidi. 

Watu wengi wana vimelea hivi katika miili yao kwa kiwango kidogo sana. Kinga ya mwili ikisaidiwa na bakteria walinzi wa mwili huweza kupambana na vimelea hivi. 

Mwanaume anapataje fangasi sehemu za siri? 
Mtu anapokunywa dawa za kuua bakteria kutokana na ugonjwa mwingine wa bakteria kama kuhara damu, husababisha bakteria walinzi wa mwili kufa, hivyo kuongeza hatari ya mwili kushambuliwa na ugonjwa wa fangasi. 

Ikiwa kinga yako ya mwili itashuka kutokana na maradhi kama VVU/UKIMWI au lishe duni pia mwili wako utakuwa katika hatari zaidi ya kupata maradhi ya fangasi. 

Hata hivyo, maradhi ya fangasi yanaweza kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwingine kwa kuchangia nguo au vifaa vya kuogea na kujamiana na mtu mwenye ugonjwa wa fangasi. 

Wanaume wengi wanaosumbuliwa na fangasi sehemu za siri huishi maeneo yenye joto sana kama Pwani, Lindi, Mtwara, Tanga na Dar es salaam. 

Kuishi sehemu yenye joto pamoja na kuvaa nguo za kubana hasa zisizo tengenezwa na pamba kwa asilimia 100 kunafanya sehemu za siri kuwa na unyevunyevu, hivyo kutengeneza mazingira mazuri kwa fangasi kuzaliana na kuongezeka. 

Dalili za fangasi sehemu za siri za mwanaume ni zipi? 
Sehemu za siri za mwanaume hata ndani ya uume, korodani, eneo katikati ya makalio na kuzunguka korodani hadi kwenye mapaja huathirika na ugonjwa wa fangasi. 

Kichwa cha uume hubadilika na kuwa chekundu na kuwasha. Ngozi inayozunguka sehemu za siri huwasha, kukakamaa na kutoa majimaji ambayo hutoa harufu mbaya. 

Matibabu ya fangasi sehemu za siri za mwanaume ni yapi? 
Ikiwa una dalili za ugonjwa wa fangasi ni vyema kufika kwa daktari kwa ajili ya matibabu na ushauri zaidi. 

Kutumia dawa bila ushauri wa daktari kunaweza sababisha kutopona kabisa, kutopona vizuri au ugonjwa kujirudia baada ya siku chache, pia vimelea vinaweza kujenga usugu wa dawa. 

Kumwona daktari kutasaidia kujua kama una maradhi mengine yanayosababisha upate fangasi sehemu za siri. 

Ugonjwa wa fangasi usipotibiwa husambaa kwenye damu na kusababisha madhara makubwa mwilini kama kwenye ubongo na mapafu. 

Mwanaume atajikinga vipi na fangasi sehemu za siri? 
Ili kusaidia kuepuka kupatwa na fangasi sehemu za siri ni vyema kuosha vizuri uume, na kwa wale ambao hawajatahiriwa wanapaswa kuosha kwa umakini zaidi hadi sehemu za ndani za govi. 

Ziweke sehemu zako za siri pamoja na ndani makalio katika hali ya usafi na ukavu, kwa maana unyevunyevu unaweza sababisha maambukizi. 

Matumizi ya poda maalumu yanaruhusiwa hasa kipindi cha joto kali ili kuzuia unyevunyevu. 
Vaa nguo isiyobana sana, iliyotengenezwa kwa vitu asilia kama pamba. Badili nguo ya ndani (chupi) angalau kila siku na vaa kondomu kila unapofanya ngono na mwanamke usiyejua hali yake kiafya kwa ujumla.

0 comments:

Banner1

Banner1