Fahamu faida na hasara za kurudiana na mpenzi wako wa zamani


NI IJUMAA nyingine tunapokutana jamvini! Shukrani za kipekee kwa Muumba wetu kwa kutuwezesha kuiona siku hii ya leo. Najua ni wengi walitamani kuiona lakini hawajafanikiwa. Nakukaribisha kwa moyo mkunjufu kwenye jamvi letu tujadiliane na kuelimishana mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi.

Bila shaka unawajua watu ambao walikuwa wakiishi pamoja kimapenzi, iwe ni ndoa, uchumba au uhusiano wa kawaida ambaowamewahi kutengana na baadaye wakarudiana, iwe ni mara moja au zaidi.

Yawezekana hata wewe ukawa miongoni mwa watu wa aina hiyo; kwamba uliwahi kutengana na mtu umpendaye lakini baadaye ukajikuta unarudiana naye na kuanzisha upya uhusiano. Je, kuna faida na madhara gani kwa wapenzi kuachana kisha kuja kurudiana tena na kuanzisha upya uhusiano wa kimapenzi? Ukiwaona watu wanaoishi kwenye aina hii ya uhusiano wa kimapenzi unawachukuliaje?

NI JAMBO LA KAWAIDA KATIKA MAPENZI
Yawezekana aina hii ya uhusiano wa kuachana na kila mmoja akaendelea na maisha yake kisha baada ya muda mkarudiana tena, likaonekana jambo la ajabu au geni katika mila na desturi za Kiafrika lakini kwa taarifa yako, hili ni jambo la kawaida kabisa katika uhusiano wa kimapenzi duniani kote.

Takwimu zinaonesha kwamba asilimia kubwa ya wanandoa au watu ambao wapo kwenye uhusiano imara wa kimapenzi, wamewahi kupitia kipndi hiki kigumu cha kutengana na kurudiana, wengine wakifanya hivyo mara kadhaa.

Wapo baadhi ya watu ambao baada ya kutengana, hushindwa kukaa chini na kumaliza tofauti zao hata kama bado wanapendana kwa kuona jamii itawashangaa kuwaona wakiwa pamoja tena baada ya kuachana kwa kashfa na vurugu kubwa. Kama na wewe ni miongoni mwa watu wa aina hii, narudia kukusisitiza kwamba hilo ni jambo la kawaida na linafanyika duniani kote.

MADHARA YAKE
Yapo madhara mengi yanayowakumba watu wanaoishi kwenye aina hii ya uhusiano. Inapotokea mmeachana na kila mmoja akaanzisha ukurasa mwingine wa mapenzi, lazima atakutana na mazingira tofauti kabisa na yale mliyozoea kuishi pamoja.

Endapo atakutana na mtu mwingine ambaye amekuzidi vitu vingi, hata ikitokea wakaachana na akarudi kwako, hawezi kukupenda kwa kiwango kile kama ilivyokuwa mwanzo kwa sababu tayari kuna vitu vipya vimeingia ndani ya kichwa chake na huo utakuwa ufa mwingine ambao siku za usoni utasababisha muachane tena.

Upo ushahidi wa wapenzi ambao baada ya kutengana na watu waliokuwa wanawapenda mwanzo, walikutana na watu wengine wenye uwezo wa kuwaridhisha na kuwafurahisha faragha kuliko ilivyokuwa kwenye uhusiano uliovunjika. Inapotokea ukarudiana na mpenzi wa aina hii, ambaye tayari ameshauona ulimwengu mwingine wa kuridhishwa kimapenzi ambao kwako hakuwahi kuuona, kamwe hawezi kutulia na wewe. Hesabu maumivu.

Suala jingine ni maradhi. Katika dunia iliyochafuka kama hii tunayoishi, ni hatari kurudiana na mwenzi wako kwa sababu hujui baada ya kutengana na wewe alikuwa akitoka na nani. Ni rahisi kukuletea maradhi ya zinaa au Ukimwi hasa kama alikuwa anatoka na watu wasio sahihi. Unapaswa kuwa makini katika hili.

Kulipizana visasi ni tatizo jingine linaloweza kuwakumba watu wanaoishi kwenye uhusiano wa aina hii. Yawezekana wewe ndiye uliyemuumiza mwenzi wako wakati mnaachana, ukautesa moyo wake na kushindwa kumuonea huruma wakati akiteseka. Inapotokea mmerudiana, wengi hubaki na vinyongo ndani ya mioyo yao na kwa sababu wewe ndiye uliyemuumiza, na yeye atakutafutia sababu ya kulipa kisasi ili na wewe uhisi maumivu kama aliyoyahisi yeye wakati mnaachana.

Hata hivyo, kama nilivyosema awali, suala hili siyo geni na linafanyika dunia nzima. Licha ya kueleza hasara zake, lazima zipo faida na ndiyo maana watu wanaendelea kuachana na kurudiana. Je, kuna faida gani kuishi katika uhusiano wa aina hiyo? Usikose kuungana nami wiki ijayo tuangalie faida zake.

0 comments:

Banner1

Banner1